MSANII wa filamu, Wema Sepetu ambaye
anatarajiwa kuchapana makonde na Jacqueline Wolper katika pambano la
utangulizi kesho, amesema sasa amekwiva na yuko fiti kutokana na mazoezi
ambayo anapewa na kocha wake Rashidi Matumla.
Akizunguza na gazeti hili jana, Wema
alisema ametumia muda mwingi katika mazoezi hivyo kesho ni lazima
atampiga Wolper kwa ‘knock out’.
“Kwa
kweli nimejifua vilivyo lengo likiwa ni kuhakikisha naweka historia
kesho ya kumchakaza Wolper, kwa nilivyo fiti sidhani kama atafikisha
raundi ya pili,” alisema Wema.
Wakati
Wema akisema hayo, Wolper amejigamba kwa kusema: “Wema ajiandae tu kwa
kipigo, ameshasema mengi ila mimi siku hiyo nataka nimfundishe adabu.
Nitamvuruga, nitampiga na kwa uzito wa ngumi nitakazomtupia asipotoka
manundu labda awe amechanjia.”
Warembo
hao wamesema kuwa wanapigana kumaliza ubishi wa muda mrefu, vilevile
kuchangia fedha Mamlaka ya Elimu Tanzania ili kuwasaidia wanafunzi wa
kike kupata mabweni na kusoma katika mazingira mazuri.
Mratibu
wa tamasha hilo, Luqman Maloto amesema kuwa Wolper na Wema kila mmoja
anatamba kumpiga mwenzake, hivyo akataka mashabiki wao kuhudhuria Uwanja
wa Taifa ili kumuona mbabe kati ya wawili hao.
“Tumekubaliana
kwa kufuata misingi yote. Wolper na Wema wameridhia kupambana ili
kumaliza ubishi na kuchangia elimu,” alisema Luqman na kuongeza:
“Wolper
na Wema wataingia uwanjani kwa helikopta. Tunatambua thamani ya Wema na
Wolper kijamii, kwa hiyo hatutaki wapitie njia ambazo zitawafanya watoe
kisingizio. Tutawaingiza kwa helikopta, kila mtu na ya kwake ili
watakapokuwa wanaingia, uwanja mzima ushuhudie.”
Luqman
aliendelea kusema kuwa pambano la Wema na Wolper litakuwa la
utangulizi, kabla ya mabondia wakubwa nchini, wenye rekodi nzito, Japhet
Kaseba na Francis Cheka kupambana kwenye pambano la kumaliza ubishi.
“Kama
nilivyokwishasema kabla, siku ya Tamasha la Usiku wa Matumaini ni
nzito. Matukio ni mengi, vilevile kutakuwa na mechi ya wabunge Simba na
Yanga, Bongo Fleva dhidi ya Bongo Movie, bila kusahau siku hiyo tutajua
mkali wa steji ni nani kati ya Jose Chameleone wa Uganda na Diamond
Platnamz wa Tanzania.
“Kutakuwa
na shoo nyingine kali kutoka kwa Roma, Chidi Benz, Juma Nature, Pah One,
FM Academia, East African Melody na wengine wengi,” alisema.
7
No comments:
Post a Comment