Stori: Gladness Mallya na Erick Evarist
SIKU chache baada ya baba mzazi wa kachala wa Bongo Fleva, Nasibu
Abdul Juma ‘Diamond Platnum’, mzee Abdul Juma kufunguka kuwa mwanaye
huyo hamthamini toka amepata mafanikio, watu waliodai wao ni ndugu wa
tumbo moja na mkali huyo wa muziki wa kizazi kipya wameibuka na kusema
baba mzazi wa Diamond alishafariki dunia mwaka 2004, Ijumaa Wikienda
lina ripoti kamili.
CHANZO CHATIRIRIKA
Baada ya habari ya kuibuka
kwa baba wa Diamond kuchapishwa kwenye gazeti ndugu la hili (Amani)
mwishoni mwa wiki iliyopita, chanzo makini kiliwatonya mapaparazi wetu
kuwa baba aliyejitokeza (Abdul Juma) siyo wa damu.
“Jamani nyie Amani
mmeandika baba wa Diamond ni mzee Abdul Juma, mbona tunavyojua sisi,
baba wa Diamond anaitwa Salum Idd na alishafariki dunia tangu mwaka
2004, kama mnataka ukweli zaidi fuatilieni,” kilisema chanzo hicho huku
kikiahidi kutoa ushirikiano.
MAPAPARAZI WAINGIA KAZINI
Mapaparazi
wetu walianza kazi ya kufuatilia nyeti hiyo ambapo kwa msaada wa chanzo,
Julai 12, mwaka huu walifanikiwa kutinga nyumbani kwa msichana aliyedai
ni dada kwa baba mmoja na Diamond.
Msichana huyo anaishi Kariakoo,
jijini Dar es Salaam na mdogo mwingine wa Diamond aitwaye Idd Salum
ambaye naye anaimba kama kaka yake.
TUJIUNGE NA IDD ALIYEPO KARIAKOO
Baada
ya salamu za hapa na pale na mapaparazi wetu kujitambulisha kwa familia
hiyo, lilifuata swali kama kweli wao ni ndugu wa damu moja na Diamond.
Idd:
“Mbona kila kitu kipo wazi, hata yule mzee Abdul Juma anaelewa kila
kitu kwamba sisi na Diamond ni ndugu, Diamond ni kaka yetu na amekuwa
akinisaidia mimi katika shida na raha, baba yetu alishafariki dunia
tangu mwaka 2004.
“Yeye (Abdul) ni baba mlezi tu na anafahamu wazi kuwa yeye ni baba mlezi wa Diamond na kwamba baba yetu alishatutoka.”
IDD AIBUA JIPYA
Kwa
mujibu wa mdogo huyo wa Diamond, Idd, mwaka 1989, mama Diamond (Sanura
Khassim ‘Sandra’) alipewa ujauzito na Salum (baba yake) kisha
waligombana na kuachana.
Akasema baada ya kuachana, mama Diamond
alikutana na Abdul ambaye alikubali kuwa naye kimapenzi na kuulea
ujauzito huo wa mtoto (Diamond).
Idd akasema Diamond alipozaliwa,
Abdul aliendelea kumlea mpaka alipofikisha miaka sita ndipo aliporudi
Kariakoo kwa baba yake mzazi (Salum) hadi alipokuwa mtu mzima.
Akaongeza:
“Alipokuja hapa, tuliendelea kuishi naye hadi alipopata uelewa wa
kuanza kufanya shuguli zake za muziki ilikuwa ni hapahapa.”
Kwa
upande mwingine, Idd alisisitiza kuwa siku zote anamtambua mzee Abdul
kama baba mlezi wa Diamond ingawaje pia anautambua mchango wake kwa
kumlea ndugu yake huyo lakini akasisitiza kuwa Abdul siye baba mzazi wa
nyota huyo.
Kijana huyo aliendelea kuweka wazi kwamba, kwa upande wa baba yao huyo marehemu, walizaliwa sita lakini kwa mama tofautitofauti.
KWA NINI NASIBU ABDUL?
Aidha, Idd hakusita kuweka wazi ni kwa nini kaka yake anatumia jina la baba mlezi, Abdul badala ya lile la baba mzazi, Salum.
“Kutokana
na Abdul kumlea Diamond tangu akiwa tumboni kwa mama yake na pia ndiye
aliyempa jina la Nasibu ndiyo maana akaendelea kulitumia jina la baba
mlezi maana lipo hata kwenye cheti chake cha kuzaliwa, hivyo ilikuwa
vigumu kubadilisha,” alisema.
KAMA NI KWELI, VIPI KUHUSU QUEEN DARLEEN?
Kama
madai hayo ni sahihi, ina maana yule msanii wa Bongo Fleva, Mwanahawa
Abdul Juma ‘Queen Darleen’ ambaye wengi wanajua yeye na Diamond ni damu
moja kwa baba, kumbe hawana uhusiano wowote ule.
KWA NINI?
Kwa
sababu kama mzee Abdul Juma alilea ujauzito wa Diamond lakini damu si
yake huku ikijulikana wazi kwamba yeye ni baba mzazi wa Queen Darleen,
kwa hiyo Diamond hachangii popote na msanii huyo wa kike.
USHIRIKIANO UKOJE?
Kijana
huyo aliendelea kutiririka kuwa, maisha yao na Diamond ni safi kwani
kunapotokea tatizo lolote, msanii huyo anashiriki kikamilifu na kila
Mwezi Mtukufu wa Ramadhan unapowadia, staa huyo huwa anakwenda kufuturu
Kariakoo hadi mfungo unapoisha.
MSIKIE TENA MZEE ABDUL JUMA
Baada
ya maelezo hayo ya Idd, kwa mara nyingine mapaparazi wetu walimtokea
mzee Abdul Juma anayedaiwa ni baba mlezi tu na kumwambia kila kitu
kuhusu maneno yaliyotoka kinywani kwa Idd.
Mzee Abdul: “Nilijua tu
kwamba kuna watu wataibuka wakidai Diamond ni mtoto wao. Hii yote ni kwa
sababu ya mafanikio aliyonayo kwa sasa, ukweli ni kuwa yule ni mwanangu
wa damu, halali kabisa. Hao wanaosema ni mtoto wao, ni matapeli.”
MAMA DIAMOND AMUNG’UNYA MANENO
Katika
hali ya kawaida, mama Diamond (Sandra) ndiye mwenye uhakika wa baba wa
mtoto huyo, hivyo Julai 12, 2012, mapaparazi wetu walifika nyumbani
kwake, Sinza-Mori, Dar ili kumsikia anasemaje kuhusu hilo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamke huyo hakuwa tayari kujibu swali lolote kuhusu Abdul Juma wala Salum Idd.
“Sitaki
kusema. Sitaki kujibu chochote. Kwa nini msimuulize Diamond, mimi na
vyombo vya habari wapi na wapi jamani? Muulizeni mwenyewe Diamond.
Paparazi: Lakini unawafahamu hawa watu, mzee Abdul na…”
Mama Diamond: (huku akiangalia ukutani) nimesema sijibu chochote. Kwa nini sieleweki?
DIAMOND, JANA KAMA JUZI
Baada
ya majibu ya kuzodoa ya mama huyo, Diamond alipigiwa simu, lakini kama
ilivyokuwa kwenye habari ya kwanza ya BABA DIAMOND AIBUKA, ANENA MAZITO
ambapo alipigiwa simu mara kumi na mbili lakini hakupokea, safari hii
pia hakupokea licha ya kutwangiwa mara kadhaa.
Mpaka gazeti hili
linakwenda kukatiza mitamboni, jitihada za kumpata Diamond kuongelea
jambo hilo ziligonga mwamba. Hata hivyo, jitihada za kumpata msanii huyo
mwenye mafanikio makubwa Bongo zinaendelea.
WASOMAJI WETU NAO WATIA NENO
Baada
ya habari ya baba Diamond kuibuka na kuchapishwa kwenye gazeti la
Amani, wasomaji walituma meseji nyingi zilizosomeka hivi: “Hili la baba
wa Diamond lina utata mkubwa, Diamond na mama yake wanatakiwa kuweka
wazi kila kitu ili kuondoa viulizo kwa jamii.
No comments:
Post a Comment