Tuesday, July 10, 2012

PIGO ZITO

Haruni Sanchawa na Makongoro Oging'
LISEMWALO lipo na kama halipo laja! Usemi huu umekamilika pale Charles Wilbroad alipopata pigo la kumpoteza mtoto wake kipenzi, Emmanuel Charles (7), siku ambayo gazeti hili liliandika habari kuhusiana na siri za Freemasons zilizotolewa na kijana huyo.
Akizungumza na gazeti hili, Charles alisema baada ya kuzungumza na mwandishi wetu kuhusiana na siri za Freemasons na kueleza jinsi alivyotakiwa amtoe kafara mwanaye, mtoto huyo alifariki dunia siku gazeti hili lilipokuwa mtaani.
“Mwanangu alifariki ghafla baada ya kuugua kwa saa mbili mfululizo kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 3:00, Jumanne ya Juni 26, mwaka huu. Madaktari walieleza kuwa kifo chake kimesababishwa na kuishiwa damu mwilini,” alisema Wilbroad.
Wilbroad aliendelea kusema kuwa kifo cha mwanaye kilimshtua sana kwani aliugua na kufa ghafla, hali aliyoitafsiri kuwa huenda ilisababishwa na imani yake ya Freemasons.
“Alianza kuumwa saa moja asubuhi, akaanguka na kupoteza fahamu. Tukamkimbiza hospitalini lakini ilipofika saa tatu asubuhi, alikata roho. Wamemnyonya damu mwanangu kwa sababu madaktari walisema ameishiwa damu,” alisema Wilbroad na kufafanua kuwa kifo hicho kiliwashitua wengi waliokuwa wakimfahamu mtoto wake huyo.
Awali, Wilbroad aliliambia gazeti hili kuwa aliwahi kuambiwa amtoe kafara mtoto wake huyo kimazingara ili maisha yake yawe mazuri lakini alikataa, badala yake akaenda kuvitupa baharini vitu alivyopewa kufanyia ushirikina huo baada ya kushindwa masharti.
Alivitaja vitu hivyo ambavyo alipewa na mtu mmoja ambaye anaishi Uarabuni (Dubai) mwaka 2009 kuwa ni pamoja na mkufu, pete pamoja na fomu maalum aliyoijaza ambayo ilieleza pamoja na mambo mengine kwamba akifa, mrithi wake angekuwa mtoto wake aitwaye Emanuel ambaye sasa ni marehemu.
Maziko ya kijana Emmanuel yalifanyika katika Kata ya Nyamililo, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza Juni 27, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment