Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na wahariri Ikulu jana.
HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 JULAI, 2012
Ndugu Wananchi;
Naomba
nianze kwa kuomba radhi kwa kutoa hotuba ya mwisho wa mwezi wa saba,
leo tarehe 01 Agosti, 2012 badala ya jana tarehe 31 Julai, 2012. Hii ni
kwa sababu ya msiba uliotukuta katika familia na mimi kwenda Lindi
kushiriki maziko ya marehemu wetu. Tofauti na miezi iliyopita leo,
pamoja na hotuba ya kawaida ya mwisho wa mwezi nimetoa fursa kwa
Wahariri wa vyombo vya habari nchini kuniuliza maswali nami kujibu. Kwa
upande wangu nina mambo matatu ambayo nitayazungumzia leo.
Ajali ya Kuzama kwa Meli ya MV SKAGIT
Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ni ajali ya Meli ya MV SKAGIT iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012. Meli hiyo ilikuwa na watu290, wakiwemo mabaharia 9, abiria watu wazima 250 na watoto 31.
Juhudi za uokoaji zilianza mara baada ya taarifa ya kuzama kwa meli
hiyo kupatikana. Maofisa na askari wa JWTZ, Polisi na KMKM walishiriki
pamoja na meli na watu binafsi katika uokoaji. Waokoaji walifanikiwa
kuwapata ndugu zetu 146 wakiwa hai na maiti 126 hadi
tarehe 27 Julai, 2012. Kwa maana hiyo basi, watu 18 hawajulikani walipo
na inahofiwa kuwa nao pia hawako hai. Huenda wamezama pamoja na meli
au walizama baharini lakini miili yao haikuweza kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kurudia kutoa mkono wa rambirambi na
pole nyingi kwa wale wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika
ajali ile. Nampongeza sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wenzake wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kazi kubwa na nzuri waliofanya
kuongoza juhudi za uokoaji pamoja na huduma walizotoa kwa waliokolewa,
waliojeruhiwa na waliofariki. Kwa wale ambao walikuwa wenyeji wa Unguja
na Pemba, SMZ ilitoa sanda na usafirishaji wa maiti mpaka makwao kwa
mazishi. Kwa wale wasiokuwa na ndugu Serikali ilibeba jukumu la
kuwazika kule Kama, Kusini Unguja.
Natoa pongezi za pekee kwa wale wote walioshiriki katika uokoaji
kwani juhudi zao ziliwezesha ndugu zetu wengi kusalimika na maiti nyingi
kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Kutokea kwa ajali ile kumetonesha jeraha la huzuni, majonzi na
mashaka makubwa yaliyolipata taifa letu miezi 11 iliyopita kufuatia
ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander. Katika mkutano maalum wa
Baraza la Usalama wa Taifa niliouitisha tarehe 20 Julai, 2012
kuzungumzia ajali ya MV SKAGIT tulifanya mapitio ya utekelezaji wa
maagizo yetu ya mkutano wa tarehe 11 Septemba, 2011 kufuatia ajali ya MV
Spice Islander. Kwa ujumla tumeridhika kuwa utekelezaji umekuwa mzuri
kwa upande wa mamlaka zinazohusika na usafirishaji majini yaani SUMATRA,
Zanzibar Maritime Authority na mamlaka za Bandari za nchi zetu mbili.
Ushirikiano baina ya mamlaka hizo sasa ni mzuri kwa mambo yote muhimu
ambayo Baraza liliagiza wafanye hivyo. Pamoja na hayo Baraza limetaka
ushirikiano huo uzidishwe na kuimarishwa.
Kwa mfano, Baraza limefurahishwa na kupongeza kitendo cha mamlaka
hizo kutumia Dar es Salaam Maritime Institute kwa ushauri kuhusu ubora
wa meli na huduma za usafirishaji majini. Baraza limeagiza vyombo
hivyo viwe na hadidu za rejea zinazofanana kwa vigezo vya ubora ili nchi
yetu iwe na viwango vinavyofanana vya ubora wa meli na huduma za
usafirishaji baharini kwa pande zetu mbili za Muungano. Bahari ni moja
na vyombo vinahudumia watu wale wale, kuwa na vigezo tofauti vya ubora
wa meli na viwango vya huduma ni jambo lisilostahili kuwepo tena, ni la
hatari. Baraza pia limeagiza pawepo na ukomo wa umri wa meli
zilizokwishatumika zinazoruhusiwa kutumika hapa nchini.
Aidha, Baraza limerudia kuagiza pawepo na usimamizi makini zaidi
kuhusu upakiaji wa mizigo na abiria. Mamlaka husika, yaani SUMATRA, ZMA
na maofisa wa bandari wahakikishe kuwa uwezo wa meli uliohakikiwa na
kutambuliwa unaheshimiwa ipasavyo. Pia, meli zikaguliwe mara kwa mara
na vigezo vifanane.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na hayo, Baraza la Usalama wa Taifa limeona kuwa wakati
umefika kwa Serikali yetu kuwa na Coast Guards, yaani kikosi maalum cha
uokoaji na usalama majini. Aidha, Baraza limetaka hatua za makusudi
zichukuliwe kuimarisha KMKM na Police Marines. Mwisho, Baraza
lilipongeza uamuzi wa SMZ wa kuunda Tume ya kuchunguza ajali ile kama
ilivyofanya wakati wa ajali ya MV Spice Islander.
Utafutaji na Uchimbaji Gesi Nchini
Ndugu Wananchi,
Jambo la pili ninalopenda kulizungumzia leo ni kuhusu maendeleo ya
sekta ya gesi asili nchini. Juhudi za kutafuta mafuta nchini zilianza
mwaka 1952 na mwaka 1954 wakati kampuni ya BP ilichimba kisima cha
kwanza kule Mafia. Bahati mbaya kisima hicho hakikuzaa matunda
yaliyotarajiwa na juhudi za utafutaji mafuta zikafifia kabisa mwanzoni
mwa miaka ya 1960. Miaka kumi baadae, juhudi hizo zilianza upya na
kuendelea kwa kiwango na kasi za namna mbalimbali hadi sasa. Katika
miaka ya hivi karibuni juhudi zimekuwa kubwa na kuhusisha makampuni
kadhaa ya kimataifa yakiwemo makubwa na madogo.
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka 1954, mpaka sasa visima 61vimechimbwa, kati ya hivyo, gesi asili imegunduliwa katika visima 22, visima 14 vya nchi kavu na maeneo ya maji mafupi na visima 8 vya
bahari ya kina kirefu. Hatujabahatika kupata mafuta lakini
tumefanikiwa kupata gesi asili katika maeneo kadhaa baharini na nchi
kavu katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kutokana na visima vilivyochimbwa
mpaka sasa, akiba ya gesi asili iliyopo nchini inakadiriwa kuwa kati ya
futi za ujazo trilioni 25.4 – 28.9. Yapo matumaini makubwa ya
gesi nyingi zaidi kugundulika katika miaka michache ijayo. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba shughuli za utafutaji mafuta na hasa gesi
baharini zilizoanza mwaka 2004 kukiwa na kampuni moja sasa zipo 18.
Baada ya ugunduzi wa kwanza wa gesi mwaka 2010, shughuli za utafutaji
sasa zimepamba moto na zimekuwa na mafanikio. Naamini gesi nyingi zaidi
itaendelea kupatikana.
Fursa za Maendeleo
Ndugu Wananchi;
Kwa kiasi cha gesi asili kilichokwishagunduliwa na kwa
matumaini yaliyopo ya gesi zaidi kupatikana kunaifanya Tanzania kuwa
moja ya nchi za kutumainiwa duniani kwa upatikanaji wa gesi asili miaka
michache ijayo. Hali hiyo inaipa nchi yetu fursa kubwa ya kuweza
kujiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii muda si mrefu kutoka
sasa.
Gesi asili ni rasilimali inayoweza kutumika kuzalisha
mbolea na hivyo kusaidia katika kuendeleza kilimo nchini kwa kurahisisha
upatikanaji wake na kuwa ya bei nafuu. Gesi asili inaweza kutumika
kuzalisha umeme na hivyo kuiwezesha nchi kupata umeme wa kutosha na
kuwepo ziada ya kuuza nje. Hivi sasa, katika gridi ya taifa megawati 350 za umeme zinatokana na gesi asili na hata lengo letu la kuzalisha megawati 3,500 ifikapo
maka 2015 tunategemea zaidi gesi asili kuwezesha hilo kutimia. Ujenzi
wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam una shabaha hiyo.
Ndugu Wananchi;
Vile vile, gesi asili inaweza kutumika kutoa nishati
viwandani badala ya kutumia mafuta na hivyo kupunguza gharama za
uzalishaji. Watu majumbani wanaweza kutumia gesi asili kupikia hivyo
kupunguza matumizi ya umeme, mafuta, mkaa na kuni. Inapunguza gharama
za maisha na kusaidia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa
miti. Ni kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana TPDC inatekeleza
mradi wa kutengeneza gridi ya mabomba ya kusambaza gesi majumbani katika
jiji la Dar es Salaam.
Jambo lingine muhimu kuhusu rasilimali hii ni kwamba
tukiuza nje gesi nchi yetu itapata mapato mengi tena ya fedha za
kigeni. Kwa vile gesi ni nyingi mapato ya Serikali yataongezeka sana,
hivyo kuijengea uwezo wa kutimiza majukumu yake vizuri zaidi. Kama
matumizi yatakuwa mazuri, gesi asili itakuwa kichocheo kikubwa cha
kukuza uchumi wa nchi. Maendeleo ya haraka yatapatikana na hivyo
kusaidia kuwaondoa wananchi wengi kutoka katika lindi la umaskini
tulionao sasa.
Changamoto Muhimu
Ndugu Wananchi;
Pamoja na ukweli kwamba kuwa na gesi asili nyingi kunaipa nchi yetu
fursa kubwa ya kujiletea maendeleo, zipo pia changamoto zake. Hatuna
budi kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi ili gesi iweze kunufaisha
ipasavyo nchi yetu na watu wake. Changamoto zipo nyingi lakini kubwa
zipo za namna tatu.
Changamoto ya kwanza ni ile ya kujenga uwezo wetu wenyewe wa
kudhibiti shughuli zinazofanywa na makampuni ya mafuta ili tuhakikishe
kuwa tunapata malipo yanayostahili. Inatulazimu tuwe na wataalamu wetu
wazalendo wa fani za taaluma zihusuzo gesi kama vile uhandisi, kemia,
jiofizikia, uhasibu, ukaguzi na sheria. Tusipojenga uwezo wetu wenyewe
kwenye maeneo hayo kuna hatari ya kudhulumiwa na kupata hasara. Pengine
ipo haja ya kuwa na chombo maalum kwa ajili hiyo kama tulivyofanya kwa
mafanikio kwa upande wa dhahabu.
Changamoto ya pili ni ile ya kupata Watanzania wengi wenye ujuzi na
taaluma zinazohitajika na soko la ajira la sekta ya gesi. Tusipofanya
hivyo makampuni yataajiri watu hao kutoka nje na hivyo kufanya
Watanzania kutokunufaika na fursa za ajira zilizopo.
Ndugu Wananchi,
Kwa changamoto hizi mbili, jawabu lipo kwenye elimu na mafunzo
tunayotoa kwa vijana wetu katika shule, vyuo vya ufundi na vyuo vya
elimu ya juu. Kwanza kabisa lazima tuboreshe elimu ya sayansi na
hisabati katika shule zetu za msingi na sekondari. Katika vyuo vya
ufundi tutoe mafundi mchundo wa taaluma zinazohitajika na tasnia ya gesi
na mafuta. Hivyo hivyo kwa upande wa vyuo vikuu nako wafundishe
wataalamu wa fani zinazohitajika kama vile utafutaji wa gesi na mafuta,
uendelezaji wa mafuta na gesi, uchumi na biashara ya mafuta na gesi,
uhasibu na ukaguzi wa mafuta na gesi pamoja na sheria za mafuta na gesi
na mikataba ya utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa tayari tumejipanga kutafuta ufumbuzi wa
changamoto hizo. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinajiandaa kuanza kutoa
mafunzo yaChemical and Environmental Lab for Oil and Gas na fani yaExploration and Production Software Technology katika mwaka huu wa masomo. Chuo cha Madini Dodoma kitaanza kutoa mafunzo ya diploma ya Petroleum Geoscience kuanzia
Septemba mwaka huu. Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Sayansi na
Teknolojia cha Nelson Mandela Arusha, na Chuo cha Teknolojia cha Mbeya
na kile cha Dar es Salaam pia wameanza kufundisha mitaala hiyo. Aidha,
VETA Makao Makuu na VETA Mtwara nao wanafundisha masomo yahusuyo gesi.
Wizara ya Nishati na Madini itawadhamini wanafunzi 50 kutoka Mkoa wa Mtwara kwenda kupata mafunzo hayo ya gesi asili katika chuo cha VETA Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Wizara ya Nishati na Madini pia inatekeleza mpango mkakati wa
kuwapata wataalamu wa sekta hiyo kati ya 40-50 kati ya sasa na mwaka
2016. Taaluma zinazotiliwa mkazo ni Petroleum Geoscience, Petroleum
Geophysics, Petroleum Geochemistry, Petroleum Engineering, Petroleum
Modeling, Oil and Gas economics, Oil and Gas Accounting and Auditing na
Oil and gas Legal Regimes and Contract Negotiations. Kwa upande
wake, Serikali itatoa upendeleo maalum kwa kulipia gharama zote za
mafunzo ili tuweze kuwapata wataalamu hawa mapema iwezekanavyo. Nawaomba
vijana wetu wachangamkie fursa hizi za masomo na watakapohitimu mafunzo
wawe tayari kuitumikia nchi yetu kwa bidii.
Kujenga Uwezo Wetu wa Kutumia Mapato ya Gesi
Ndugu Wananchi,
Changamoto nyingine kubwa sana ni ile ya kuhakikisha kuwa mapato
yatokanayo na gesi yanatumika vizuri na kwa manufaa ya taifa na watu
wake. Lazima tuanze sasa kufikiria na kujipanga kwa ajili hiyo. Si
vyema tukangojea mpaka hapo mapato yatakapoanza kupatikana ndiyo
tufikirie na kutengeneza mfumo mzuri wa kusimamia na kutumia mapato
yatokanayo na gesi. Tutakuwa tumechelewa, watu laghai na waovu watakuwa
wameanza kunufaika hivyo watakuwa wagumu kutengeneza mfumo
utakaowanyima fursa ya kuliibia taifa.
Jambo hili ni muhimu sana kufanya kwani ipo mifano hai ya nchi
zenye rasilimali nyingi za mafuta na gesi lakini nchi na wananchi wake
hawanufaiki sawia. Mauzo yanafanyika na fedha nyingi kupatikana lakini
manufaa kwa nchi na watu wake ni madogo au hayapo kabisa. Wanaonufaika
ni viongozi na baadhi ya maofisa wa umma wanaohusika na usimamizi wa
shughuli zihusuzo rasilimali hizo. Na, hata sisi tunaweza kujikuta
katika hali hiyo kama tusipojipanga vizuri sasa ambayo badala ya
rasilimali kuwa baraka zinageuka kuwa balaa au hata laana.
Ndugu Wananchi;
Zipo nchi duniani ambazo zina usimamizi mzuri wa mapato ya
rasilimali za mafuta na gesi na kuleta baraka na neema kwa taifa na watu
wake. Nchi hizo zimeweza kuhifadhi na kutumia vizuri mapato yake
kukuza uchumi wa nchi kwa jumla na kuboresha upatikanaji wa huduma za
kiuchumi na kijamii kwa watu. Matokeo yake ni watu wa nchi hizo kuishi
maisha yaliyo bora kuliko walivyokuwa kabla ya kupatikana kwa rasilimali
hizo. Lakini, hii imewezekana kutokana na usimamizi mzuri na matumizi
mazuri ya mapato yatokanayo na mafuta na gesi.
Tumeamua kujifunza kutoka nchi za wenzetu waliofanikiwa ili na
sisi tunufaike. Na sisi tunajiandaa kutengemeza Sera ya Gesi Asili na
kurekebisha Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta na Sheria ya
Menejimenti ya Mapato ya Serikali yatokanayo na gesi zitakazotoa majibu
hayo na kuliwezesha taifa kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa utafutaji
na uchimbaji wa gesi asili pamoja na usimamizi na matumizi mazuri ya
mapato yatokanayo na gesi hiyo. Wapo wenzetu kwa mfano, wanacho kitu
kinachoitwa Sovereign Funds ambapo mapato yote huhifadhiwa
na baadae hutolewa kwa utaratibu maalum. Tunataka tujifunze kutoka
kwao ili na sisi tutengeneze chombo chetu cha namna hiyo ili tunufaike.
Ndugu Wananchi;
Mambo hayo tumeshaanza kuyafanyia kazi. Katika mazungumzo yangu na
baadhi ya wakuu wa nchi rafiki na mashirika ya maendeleo ya kimataifa,
nimewasilisha maombi ya kusaidiwa na kushirikiana kwa mambo mawili.
Kwanza kwa kuwawezesha Watanzania kupata mafunzo ya haraka kwa wataalamu
watakaosaidia kusimamia shughuli za utafutaji, uendelezaji na biashara
ya gesi asili nchini. Pili, watusaidie kupata watu wenye ujuzi na
uzoefu ili watushauri kuhusu namna ya kutengeneza mifumo bora ya
kusimamia na kutumia mapato ya gesi kwa mujibu wa mifano ya wenzetu
waliofanikiwa. Nafurahi kwamba maombi yetu yamepokelewa vizuri na nchi
zote na mashirika yote ya kimataifa tuliozungumza nao. Baada ya muda si
mrefu kazi itaanza.
Mgomo wa Walimu
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu na la mwisho ni mgomo wa walimu. Pengine
ni mapema kusema kwa vile kesho Mahakama itaamua kuhusu shauri hilo.
Lakini napenda kuwahakikishia walimu kuwa tunawajali, tunawathamini na
kutambua mchango wao muhimu kwa taifa letu. Wakati wote tumekuwa
tunashughulikia madai ya haki zao na malimbikizo mbalimbali. Madai ya
safari hii ni makubwa mno, yametuzidi kimo. Athari za kuyatimiza
yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali kutumia asilimia 75kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na kubakiza asilimia 25 kwa
kuendeshea Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi.
Haitakuwa sawa. Ndiyo maana tumeshindwa kuelewana walipokataa rai hiyo
na wao kusisitiza kugoma.
Wakati tunaendelea kusubiri uamuzi wa Mahakama, nina maombi mawili
kwa walimu: Moja, wasiwalazimishe walimu wasiotaka kugoma wafanye
hivyo, wawaache waendelee na kazi. Pili, wasitumie watoto isivyostahili
kujenga hoja zao. Nawasihi warudi kwenye meza ya mazungumzo.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu naomba nitumie fursa hii kuwatakia
Waislamu wote nchini kheri na baraka tele kwa swaumu ya mwezi mtukufu wa
Ramadhan. Wakati wote, mjiombee wenyewe kwa Mwenyezi Mungu awajaalie
toba na malipo mema katika mfungo huu. Mkumbuke pia kuiombea nchi yetu
amani, upendo na mafanikio mema.
Baada ya maneno hayo, naomba sasa niishie hapo. Nawashukuru sana kwa
kunisikiliza. Sasa nipo tayari kujibu maswali ya Wahariri kama yapo.
Ndugu Wahariri mliopo hapa, karibuni.
No comments:
Post a Comment