Tafadhali husika na kichwa cha habari hapo juu.
Sisi Madiwani wa CHADEMA tumefikiri
na kutafakari kwa kina kuhusu mustakabali wa maendeleo ya wananchi wa
Manispaa ya Arusha Mjini. Kwa nafasi yetu ya wawakilishi na utetezi wa
wananchi Arusha kwa umoja wetu ni vema tufikiri na tutafakari kwa kina
kwa pamoja hasa kipaumebele ikiwa ni kutanguliza HAKI na MAENDELEO
katika kumlenga kila mkazi wa aliyepo katika Halmashauri yetu. NI vema
tukawa WAKWELI na WAZELENDO kwa wananchi wetu wa Arusha, huku wote
tukijua kwa kina kile kilichotokea Arusha.
Kwa muda mrefu kumekuwa na
mgogoro wa Uchaguzi wa MEYA wa manispaa ya Arusha, ambayo ilitokana na
ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi wa Meya ambayo akidi yake
ilikuwa haijatimia. Ikumbukwe kuwa Mhe. Kivuyo ambaye katika sakata hilo
alijikuta akichaguliwa kwa hila kuwa NAIBU MEYA, alifikia hatua ya
kujizulu nafasi hiyi na kukiri mbele ya waandishi wa habari na wananchi
wa Arusha kuwa uchaguzi uliofanyika haukuwa wa haki na yeye alipewa
nafasi hiyo kwa hila, kitu ambacho baada ya tafakari ya kina aliamua
kujiuzulu ili asiwe sehemu ya dhambi hiyo na kujikuta anakalia KITI CHA
DAMU. Jambo hili pia limekuwa likisemwa na baadhi ya madiwani wa CHAMA
CHA MAPINDUZI pindi tunapokutana nao kuwa mfumo wa chama cha CCM unazuia
kuyatamka haya lakini ukweli ni kuwa huo uchaguzi wa meya uliofanyika
na Mhe Gaudence Lyimo kupata nafasi hiyo ulikuwa batili kwa mujibu wa
kanuni, lakini mbaya zaidi, umepelekea damu kumwagika, jambo ambalo ndio
baya.
Wote tunashuhudia jinsi
ambavyo mgogoro huu ulivyo na madhara makubwa sana kwa wananchi wetu na
sisi pia ambao ni sehemu ya jamii hiyo hiyo. Mbali na kusababisha watu
watatu kupoteza maisha, pameendelea kutokea sintofahamu kubwa kutoka kwa
wananchi jambo ambalo limeendelea kuzidisha hasira kwa wananchi kwa
serikali. Jambo hili ni vema likafanyiwa kipimo maana mchezo huu na hila
hii inaweza kuzaa balaa ambalo sio rahisi kulimudu tena.
Dharau na makusudi
yanayofanywa na chama cha mapinduzi, mathalani Mhe Gaudence Lyimo na
MKURUGENZI wa halmashauri katika kupuuzia wito wa CHADEMA kuwa HAKI
haikutendeka, KANUNI zilivunjwa na hivyo uchaguzi wa MEYA ufanyike upya
kwa kufuata kanuni sasa inafika mahali haivumiliki na hapo ndipo itakuwa
mikononi mwa wananchi na sio CHADEMA tena.
Sambamba na hali hii, pia
mgogoro huu unatumiwa na watendaji wa Halmashauri kufanya mambo yao
yasiyo ya kiuadilifu kwani hakuna udhibiti wa kabisa katika uendeshaji
wa halmashauri yetu. Waheshimiwa madiwani, katika ukweli huu, MKURUGENZI
na huyo anayeitwa MEYA watatoa wapi ujasiri na kujiamini “moral
authority” ili hali wao wameshiriki dhambi mbaya ya kuchakachua kanuni
za kufanya uchaguzi wa meya isivyo halali na mbaya zaidi Mhe Gaudence
kuendelea kung’ang’ania nafasi hiyo kwa kiwango cha damu ya watu
kumwagika bila hata kujali??
Hata hivyo, hata kama Mhe
Gaudence Lyimo hatajali wito huu ambao kwetu ni wito wa mwisho kwake na
chama chake, jambo hili tunaliacha kwa MUNGU mwenye HAKI atashughulika
nae kwa wakati wake na muda si mrefu tutapata majibu ya maombi yetu.
Pili tunaliacha jambo hili kwa wananchi ili waamue kwa sababu wameshajua
wazi kuwa Mhe Gaudence Lyimo na chama chake waliamua na wameendelea
kuwafanyia uhuni katika mji wao. Sisi tumeliacha kwao waamue
watakavyoamua.
Tunafahamu kabisa katika
nafsi na mioyo yenu mnafahamu uchaguzi haukuwa halali lakini mnashindwa
kusimamia ukweli kwa sababu ya ubinafsi na kukosa uzalendo kwa wananchi
wa Arusha kwa kutanguliza maslahi yenu mbele, kitu ambacho tusingependa
kipewe tafsiri hiyo
Tunawasihi kwa dhati kabisa tuamue
kwa pamoja kwa manufaa ya Arusha tukubaliane kama viongozi wazalendo,
wapenda maendeleo na wenye hofu ya MUNGU tufanye uchaguzi wa MEYA wa
Halmashauri ya Arusha ambao utakuwa ni halali kwa vyama vyote.
Nchi nyingi za Afrika
kumekuwa na vita vya wao kwa kwao kwa sababu ya uchu wa madaraka. Hili
limetokea pia hapa Arusha watu wamekufa kwa sababu ya MEYA, hii ni aibu
na ni dhambi kwa kung’ang’ania madaraka ambayo si haki.
Waheshimiwa madiwani
wenzetu hata juhudi za serikali kufanya maendeleo wananchi wengi wa
Arusha bado hawana imani na serikali yao kwa sababu ya MEYA tu. Hivi
sasa kuna mradi wa ujenzi w barabara unaondelea ukweli ni kwamba jambo
hili ni zuri lakini wananchi wanalibeza sana kama vile linafanywa kwa
hila. Kwa nini iwe hivi??
Kimsingi tunataka MEYA
ambaye yupo huru kutembelea kata zote kwa ajili ya maendeleo bila kujali
itikadi ya chama chake. Hatutaki MEYA anayevizia misiba na harambee.
Mwisho tunamwomba Mh. Gaudence Lymo
atafakari kwa kina kwa kumuomba MUNGU wake ampe hekima na ujasiri wa
kuchukua maamuzi magumu ya kujiuzulu nafasi ya UMEYA na uchaguzi wa
kidemokrasia ufanyike kwani utampa heshima na amani katika maisha yake
yote.
Tunaomba Waheshimiwa Madiwani
wenzetu kwa pamoja tuseme dhambi hii imetosha na tutubu kwa kufanya
uchaguzi wa haki na Amani. Na kwa dhati kabisa yeyote atakayechaguliwa
hata kama ni Mh. Gaudence tutampa ushirikiano wa dhati kabisa.
Tunaomba ushirikiano wenu
katika jambo hili ambalo ni la msingi kwa maendeleo ya watu Arusha. Kila
mmoja kwa imani yake aombee jambo hili kwani halitaki ushabiki
linahitaji utulivu wa akili.
WAHESHIMIWA MADIWANI, FANYENI TAFAKARI YA
KINA, ZINGATIENI JINSI WANANCHI KATIKA KATA ZENU WANAVYOWATAZAMA, ni
matumaini yetu kuwa tutafanya uchaguzi wa MEYA ndipo tufanye uchaguzi wa
Naibu MEYA. Na jambo hili litakuwa ni ushindi na sifa iliyotukuka kwa
MADIWANI WOTE na sio kundi fulani la watu.
Asanteni sana
Doita Isaya Harri
Mwenyekiti madiwani wa CHADEMA
Nakala:
Katibu wa CHADEMA (M)
Katibu wa CCM (M)
Katibu wa TLP (M)
Mkurugenzi wa Halmashauri – Arusha Mjini
No comments:
Post a Comment