Monday, July 16, 2012

MANJI AUKWAA UENYEKITI YANGA KWA KISHINDO



                                                                         Yusuph Manji
 KLABU ya soka ya Yanga imefanikiwa kupata viongozi wapya baada ya uchaguzi uliofanyika jana na kumalizika alfajiri ya leo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam. Uchaguzi huo wa klabu hiyo ambao umekuja kufuatia aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga kujiuzulu wadhfa huo kutokana na shinikizo la wanachama wa klabu hiyo baada ya timu kuonyesha kusuasua katika Ligi Kuu Tanzania bara na kujikuta wakimaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita. Katika uchaguzi huo ambao ulishuhudia pia ukipata makamu mwenyekiti mpya baada ya`aliyekuwa akikamata nafasi hiyo Davis Mosha kujiuzulu machi mwaka jana kutokana na kushindwa kuelewana na Nchunga. Mbali ya nafasi hizo mbili pia walichaguliwa wajumbe wa watano wa kamati ya utendaji ili kuziba nafasi za wajumbe waliojiuzulu kwa nyakati tofauti katika kipindi cha Nchunga alipokuwa madarakani. Safu ya viongozi wapya wa klabu hiyo inaongozwa na mwenyekiti Yusuph Manji ambaye alijizolea kura 1876 sawa na asilimia 97 ya kura zote zilizopigwa huku wapinzani wake katika kinyang’anyiro hicho John Jambele akipata kura 40 sawa na asilimia 2.6 na Edgar Chibula aliyepata kura nne sawa na asilimia 0.24 kura zote. Nafasi ya makamu mwenyekiti mpya ilichukuliwa na Clement Sanga aliyepata kura 1948 sawa na asilimia 62.6 ya kura zote ambaye alikuwa akishindana na Yono Kevela aliyepata kura 475 sawa na asilimia 23 na Ayoub Nyenzi aliyepata kura 288 sawa na asilimia 14. Nafasi nne za wajumbe zilichukuliwa na Abdallah bin Kleb aliyepata kura 1942, Moses Katabaro kura 1068, Aron Nyanda kura 922 na George Manyama kura 682 na kukamilisha safu ya wajumbe wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment